Friday, May 4, 2018
KILIMO BORA CHA MAHARAGE
UTANGULIZI
Maharagwe (pia: maharage) ni mbegu za mimea mbalimbali (miharagwe) kutoka familia ya Fabaceae lakini mara nyingi sana Phaseolus vulgaris.
Mbegu hizi ni zao muhimu la chakula zinazolimwa kote duniani. Kuna spishi mbalimbali zinazojumlisha kati ya mazao ya jamii kunde. Mara nyingi mbegu zinavunwa baada ya kukauka na faida yake ni ya kwamba zinakaa muda mrefu, haziozi haraka.
Kuna aina zinazoweza kuliwa zikiwa bichi kabla ya kukomaa na kupikwa hivyo katika makaka yao: maharagwe-mboga. Kenya inalima aina hii kwa soko la Ulaya zikisafirishwa kwa ndege.
Maharagwe huwa na kiasi kikubwa cha protini. Kwa watu wasiokula nyama, au wana uwezo mdogo tu kujipatia nyama, maharagwe zinatosheleza mahitaji ya protini.
Asili yake
Mharagwe ni mmea ukuao kwa mwaka mmoja wenye asili ya Amerika ya Kati ya kale na huko Andes, na sasa unalimwa maeneo mengi duniani kwa mbegu zake za maharagwe zinazoliwa, zilizo maarufu zote zikiwa zimeiva na hata zikiwa bado mbichi. Tani milioni 18.3 za maharagwe makavu na nyingine milioni 6.6 za maharagwe mabichi zililimwa mnamo mwaka 2007 duniani kote. Maharagwe ni miongoni mwa vyakula vikuu vya huko Amerika.
Majani yake kwa kawaida hutumika kama mboga na mashina yake hutumika kama chakula cha wanyama.
Kitaalamu, mharagwe upo kwenye kundi la dikotiledoni. Mharagwe hupata naitrojeni kupitia vitundu vilivyopo kwenye mizizi yake, kutokana na kazi ya bakteria ziitwazo rhizobia.
Maharagwe ya kawaida ni spishi kubwa yenye historia ndefu. Mmea wake huwa na ukubwa wa sentimita 20 – 60. Aina zote hutoa majani ya kijani au zambarau, yaliyogawanyika katika sehemu tatu, kila moja likiwa na urefu wa sentimita 6 – 15 na upana wa sentimita 3 – 11. Hutoa maua meupe, ya pinki au ya hudhurungi yenye urefu wa sentimita 1, ambayo hukuwa na kuwa ganda lenye urefu wa sentimita 8 – 20. Ganda hili huweza kuwa na rangi ya kijani, njano, nyeusi au ya hudhurungi, na kila moja huwa na mbegu 4 – 6. Maharagwe huwa laini, yaliyotuna na umbo la mafigo, yakiwa na urefu mapaka wa sentimita 1.5, huku yakiwa na rangi mbalimbali, na mara nyingi huwa na mchanganyiko wa rangi mbili au zaidi.
Aina nyingine ya maharagwe ni haragwe pana, mbegu ya Vicia faba, ambayo tani milioni 3.7 tu zililimwa mwaka 2007. Biashara ya maharagwe imejigawanya vizuri katika nchi za Asia, Afrika, Ulaya, Oceania, Amerika ya Kusini na Amerika ya Kaskazini. Brazili ndiyo wazalishaji wakuu wa maharagwe makavu huku China wakiwa ndiyo wazalis
haji wakuu wa maharagwe mabichi, kwa wastani sawa na wazalishaji kumi wote waliobakia kwa pamoja.
Maharage n zao muhimu kwa chakula, lishe na kipato kwa familia na Taifa. Kwa mavuno mengi ni vizuri kuzingatia kanuni bora muhimu za kilimo bora cha Maharage. Mavuno mengi na yenye ubora huchangiwa na matumizi ya mbegu bora. Mbegu bora ni mojawapo ya pembejeo muhimu katika Kilimo. Ubora wa mbegu unatakiwa kufuata hatua zote za uzalishaji mbegu shambani, uvunaji, usafirishaji, kupakia kwenye vifaa, kufunga, usambazaji, kuhifadhi na uuzaji.
Mbegu ya kuazimiwa ubora (quality declared seed) huzalishwa na wakulima wadogo wadogo na vikundi vya wakulima wadogo vijijini, chini ya usimamizi wa washauri wa Kilimo wa Wilaya.
SIFA ZA MBEGU BORA/VIPIMO VYA UBORA WA MBEGU.
. Mbegu za aina moja (uhalisia wa kizazi) – Ili kuwa na sifa hii ukaguzi lazima uanzie kwenye shamba la kuzalisha mbegu.
. Mbegu safi – Zisizochanganyika na aina zingine au mazao mengine, mbegu za magugu, zisizoliwa na wadudu na uchafu kama udongo na takataka zingine.
. Mbegu zilizokomaa na kukauka vizuri – Kama zimekauka vizuri haziwezi kuoza na kuvunda, na huota vizuri pia haziwezi kushambuliwa na wadudu kwa urahisi. Hii huiwezesha mbegu ibaki na ubora wake kwa muda mrefu.
. Mbegu zilizovunwa kutoka mimea yenye afya kutoka shamba lenye mazao mazuri – Mbegu zilizovunwa kutoka kwenye mimea dhaifu haziwezi kuota vizuri na kwa wakati mmoja na mimea yake huwa dhaifu.
. Mbegu yenye afya nzuri – Mbegu ambayo haiwezi kuwa chanzo cha magonjwa. Fungu la mbegu isiyo salama kiafya isitumike kama mbegu. Vime vya magonjwa huweza kusambazwa kwa njia ya mbegu kama mbegu hii itatumika.
. Mbegu zenye uwezo wa kuota kwa zaidi ya asilimia tisini (90%).
. Mbegu za aina bora zinazokibalika (chagua aina ya mbegu kulingana na mahitaji).
. Mbegu mpya (pre-basic/foundation), isirudiwe kupandwa zaidi ya misimu miwili.
SEHEMU YA KUPANDA.
. Panda sehemu zenye udongo usiotuamisha maji na wenye rutuba.
. Panda mbegu katika maeneo yenye mwinuko wa mita 400m-1800m kutoka usawa wa bahari kwa nyanda za juu kusini.
WAKATI WA KUPANDA.
. Usipande kipindi cha mvua nyingi zinazoanza mwezi Novemba au Disemba hadi April au mei, panda mwezi Februari hadi March.
. Sehemu kavu zenye mvua ya muda mfupi kama, panda mwezi Disemba hadi Februari.
. Sehemu zenye maji ya umwagiliaji panda wakati wa kiangazi.
UPANDAJI.
. Panda kwa nafasi zinazoshauriwa sentimita 50 mstari hadi mstari na sentimita 10 mbegu hadi mbegu (50cm × 10cm).
. Tenga aina mbalimbali za mbegu kwa nafasi ya mita zisizopungua mita 3.
. Usipande mbegu katika mchanganyiko wa mazao mengine.
MBOLEA
. Weka mbolea wakati wa kupanda kama inavyopendekezwa. Mfano, mifuko 1 (kilo 50) TSP na 3/4 (kilo 40) mfuko CAN au DAP mfuko 1 (kilo 50).
PALIZI
Wahi palizi ya kwanza ndani ya wiki 2 baada ya maharage kuota na rudia tena kabla ya kuchanua. Unaweza kutumia madawa ya kuua magugu kama SATECA au Stomp.
WADUDU
. Funza wa maharage ni wadudu wanaoshambulia mimea michanga ya maharage. Funza wa maharage hawa huweza kusababisha uharibifu hadi kufikia asilimia 100 kufuatana na hali ya hewa-unyevu kidogo, rutuba kidogo, kuwepo kwa maotea ya aina ya maharage na magonjwa kwenye udongo, kurudia kupanda zao la maharage kila msimu na aina ya naharage.
Njia nzuri ya kudhibiti funza wa maharage haws ni:-
1. Kupanda mapema
2. Kupakaza mbegu dawa kama endosufan, Acephate, Murtano (mchanganyiko wa dawa ya fungas na wadudu) nasaidia kuzuia funza wa maharage na visababishi vya kuozesha mizizi.
TAHADHALI: Dawa ya Murtano ni sumu kali hivyo mbegu zenye dawa hii zisitumike kwa chakula.
3. Kunyunyizia dawa mfano Karate 5EC au Actellic 50EC ndani ya siku 4 hadi 5 baada ya maharage kuota.
4. Kupanda mbegu zenye afya kwenye udongo wenye rutuba.
5. Kupanda mbegu zenye ukinzani wa funza wa maharage.
6. Kuweka matandazo kama pumba ya mpunga husaidia kuotesha mizizi mipya n kurudisha afya ya mmea wa maharage.
MAGONJWA
Magonjwa maarufu ni ndui ya maharage, madoa pembe, kutu, magonjwa yanayosababishwa na bacteria na virusi. Mbegu iliyoambukizwa, udongo na takataka za maharage ni vyanzo vikubwa vya uambukizaji kwa magonjwa yote isipokuwa ugonjwa wa kutu ya majani.
1. Punguza athari kwa kupanda mbegu safi, zenye afya zisizo na vidonda/ magonjwa, aina zinazovumilia na kutunza shamba.
2. Panda kwa mzunguko wa mazao ya jamii nyingine.
3. Ondoa na kuchoma yaliyougua.
4. Tumia dawa zilizopendekezwa kama Kocide, Funguran, Bayleton n.k kwa kuzuia magonjwa yanayosababishwa na ukungu na bacteria.
KUVUNA NA KUTAYARISHA MBEGU.
Vuna maharage mar yatakapokauka. Kausha kwa kuanika juani, piga, peta na kausha tena juani. Unaweza kuvuna kilo 600 hadi 800 kwa ekari kabla ya kuchambua endapo utafuata kanuni za kilimo bora.
Chambua mbegu vizuri kwa kuondoa uchafu, udongo, mbegu za aina nyingine, punje zilizopasuka na zilizohafifu. Pia ondoa punje zenye vidonda/mabaka na zilizotobolewa na wadudu. Hakikisha mbegu zimekauka vizuri kabla ya kuhifadhi.
KUHIFADHI MBEGU.
Safisha vyombo au ghala na ondoa wadudu. Zuia wadudu kwa kutumia dawa za asili au za viwandani. Tumia dawa za kuhifadhia mbegu kama Actellic (gramu 100 za Actellic super Dust kwa kilo za mbegu za maharage), Murtano (gramu 300 za Murtano kwa kilo 100 za mbegu za maharage) na dawa zinginezo kwa kiwango kinachoshauriwa na wataalamu. Weka mbegu mbali na maharage ya chakula pamoja na vyakula vingine. Epuka sehemu zenye unyevu na paa zinazovuja na zuia panya. Usihifadhi mbegu kwa zaidi ya misimu miwili maana baada ya hapo uwezo wa kuota hupungua.
Contact/ Wasiliana nasi
Phone (Simu): +255766797400 Email: daudilyela@yahoo.com
Our Services ( Huduma zetu): Research( Utafiti), Project Proposal ( Mapendekezo ya Miradi), Business Plan ( Plani za Biashara), Profit Assessment ( Upimaji wa Faida),
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
KILIMO BORA CHA NDIZI
Ndizi ni tunda muhimu Afrika ya Mashariki na katika nchi za joto kwa jumla hasa visiwa vya caribian. Mmea wake huitwa mgomba. Kibiolojia n...
-
UTANGULIZI Tango ni zao linalopendelea hali ya hewa ya joto na husitawi vema kati ya nyuzi joto 18°C hadi 35°C Udongo Hustawi vizuri katika ...
-
UTANGULIZI Nyanya Chungu au Ngogwe ni zao la kitropic linalotoa mazao yake kama matunda na kutumika kama mboga, kuna aina mbalimbali za nya...
-
UTANGULIZI Tikiti maji ni tunda ambalo kisayansi hujulikana kama Citrullus lanatus katika familia ya Cucurbitaceae , ambalo mmea wake hutoa...
No comments:
Post a Comment