Friday, May 4, 2018

KILIMO BORA CHA MAHINDI



UTANGULIZI
Mahindi ni zao la nafaka ambalo mmea wake huna ni mrefu na hukuwa kwa mda mfupi, kitalaamu mahindi huitwa Zea mays, kuna mahindi ya aina mbalimbali kama mahindi ya bisi (Popcorn) na mahindi ya kawaida yakitofautiana rangi, kama njano, zambarau, nyeupe na nyekundu.

ASILI YAKE
Mahindi yaligundulika katika bonde la Tehuacan huko Mexico na tafiti zilizofanyika kwa sasa inasemekana na maeneo ya kusini ya kati ya bonde la mto Balsas. Kwa mujibu wa mafunzo ya kijenetiki ya Embrapa, kilimo cha mahindi kwa mara ya kwanza kilianzishwa kusini mwa Amerika kutoka Mexico miaka 5000 iliyopita na kusambaa kupitia Andes. Kwa sasa Mahindi hulimwa maeneo karibia yote duniani kwa matumizi tofauti, asilimia kubwa ya nchi za Afrika hutumia kwa chakula.

HALI YA HEWA
Mmea huu unahitaji kiwango cha joto cha kila siku cha nyuzi joto 20º ili umee vyema. Joto
la juu sana kwa mazao mazuri ni kama nyuzi joto 30º sentigredi. Katika nchi za joto jingi (tropiki), mahindi hufanya vyema katika mvua ya kiwango cha milimita 600 hadi 900 wakati wa kukua. Mahindi yaweza kukuzwa katika udongo wa Kichanga (Sand soil), Tifutifu (Loam soil), kwa baadhi ya maeneo na Mfinyanzi (Clay soil) na (PH) kutoka 5 hadi 8 ingawa 5.5 hadi 7 ndio mwafaka. Mahindi yako katika kikundi cha mimea kinachoaminika kuathirika na hali ya chumvi katika maji na udongo.

UANDAAJI WA SHAMBA
Tayarisha shamba la mahindi mara tu baada ya kuvuna mazao ya msimu uliopita maana udongo unakuwa bado mlaini na ni rahisi kulima. Mahindi hustawi sehemu yenye udongo wenye rutuba na usiosimamisha maji. Tumia mbolea za asili (samadi au mboji) ili kuongeza rutuba katika shamba lako. Moto usitumike wakati wa kuandaa shamba.

UANDAAJI WA MBEGU
Mbegu za mahindi zipo za aina mbalimbali. Panda mbegu bora: Kuna aina tatu za mbegu, chotara (hybrid), kompositi na kienyeji (asili). Sehemu za miinuko ya juu (mita 1500-2300 kutoka usawa wa bahari), UH615, UH6303, TMV-2, PAN691, H625, H614D, Seedco627 nk.
Sehemu za miinuko ya kati (100-1500) UH6303, TMV-2, SC627, Staha, Kilima nk.
Nunua kilo 10 kwa kila ekari moja, mbegu zinazobaki zitumie kurudishia ambazo hazitaota/kuharibiwa na ndege au Panya.
Nunua mbegu bora kwenye mifuko yake halisi. Pia dai risti ili uweze kuhalalisha malalamiko endapo mbegu hiyo itakuwa na matatizo baadaye.

UPANDAJI
Ni muhimu kupanda wakati mvuli pindi mvua za mwanzo zinapoanza kunyesha, Idadi ya mimea katika eneo ni muhimu kwani ikizidi Kuna uwezekano wa mazao hupungua, mmea huangushwa na upepo, mabua mengi hayazai, Idadi ya mimea nayo ikipungua kwenya eneo husababishwa mavuno kupungua.
jambo la kufanya ni kupanda mbegu katika nafasi sahihi zilizoshauriwa na mtaalamu.
MBEGU MOJA: 75sm kwa 30sm kwa kutumia mbegu moja kila shimo. Hii hutoa mimea 44,000 katika heka. Nafasi nyingine inayotumika ni 90sm kwa 25sm ambayo nayo hutoa mimea 44,000kwa hekari.
MBEGU MBILI: 90sm kwa 50sm kwa kutumia mbegu mbili katika kila shimo ambayo pia hutoa mimea 44,000 kwa hekari. Kiasi cha mbolea kwa kila shimo kinapimwa na kifuniko cha chupa ya soda.
Ushauri: Weka mbolea kwanza ndipo ufukie kidogo kabla ya kuweka mbegu, baada ya kuweka mbegu ndipo fukia.

MUDA WA KUPANDA KATIKA MIKOA YA TANZANIA
Kwa kuwa vipindi vya mvua vimetofautiana wakulima wanatakiwa kufuata majira ili kupata mavuno mengi. Angalia mapendekezo
– Iringa na maeneo ya jirani, katikati ya mwezi Novemba hadi Desemba mwishoni
– Morogoro na maeneo ya jirani, Mwezi Januari katikati hadi Februari katikati
– Mbeya na maeneo ya jirani, mwanzoni mwa mwezi Novemba hadi Desemba
mwishoni.
– Songea na maeneo ya jirani, katikati ya mwezi Novemba hadi Januari mwanzoni.
Ili kuwa na uhakika wa mavuno ya zao la mahindi unatakiwa kupanda mahindi mapema, ikiwezekana wiki moja kabla ya mvua kuanza kunyesha ila isiwe mapema sana maana mbegu zitaharibika kutokana na joto, mvua haitabiriki basi subiri mvua zianze kunyesha.
MBOLEA
Ifahamike kuwa mmea unahitaji virutubisho. Virutubisho hivyo ni pamoja na madini muhimu kama vile naitrojeni, fosfati na potasi. Madini mengine ni pamoja na salfa, chokaa, magnesium, boroni, shaba, chuma, manganese, molybedenum na zinki. Haya madini kwa asili, yanapatikana katika udongo kwa viwango tofauti.
Ushauri: Tumia mbolea za asili (samadi au mboji) pamoja na mbolea za viwandani ili kuongeza mazao. Mboji huwa haibebwi na mvua na faida yake hudumu kwa muda mrefu.

AINA KUU ZA MBOLEA
(i) Mbolea za asili mfano; samadi,mboji na majani mabichi,mbolea hizi hua na
virutubisho vya kutosha ambavyo havijulikani vipo kwa kipimo kiasi gani.
(i) Mbolea za viwandani, hizi hua na virutubisho vya kutosha na vipimo hujulikana, hii
inasaidia kujua ni kiasi gani kitumike kwa kipindi gani.
Mahindi yanahitaji rutuba na mbolea, kwa mavuno mazuri weka mbolea za asili (samadi au mboji) kipindi cha utayalishaji wa shamba. Kipindi cha kupanda kama eneo halina rutuba tumia mbolea za viwandani na kiasi cha mbolea kwa kila shimo kinapimwa na kifuniko cha chupa ya soda.
KWA MFANO:
Mbolea inayotumiwa na wakulima wadogo mara yingi huwa haitoshi. Mahindi ya kiwango
cha juu yaweza tu kufikia kiwango cha juu cha Uzalishaji iwapo yatapewa lishe na madini
ya kutosha. Mahindi ya tani 2 kwa hekta na tani 5 kwa hekta hutumia karibu kilo 60 N, kilo
10 za P205 na kilo 70 K20 kutoka katika udongo. Mahindi hunyonya Nitrogen pole pole
katika miezi ya kwanza baada ya kupanda, lakini huongezeka hadi kiwango cha juu kabisa
wakati wa kutoa maua na kukuza tunda (gunzi). Mahindi huhitaji nitrogen kwa kiwango
cha juu na ukosefu huwa ndio kizingiti. Kiwango cha juu cha nitrogen kinahitajika mara
tatu; kwanza wakati wa kupanda, pili, wakati ambapo mmea umefikia sentimita 50 za urefu
na tatu, wakati matunda ya mahindi yanaanza kutoa zile nyuzi nyuzi nyororo (silking).
Udongo mwingi huwa na madini ya phosphorous (P205) na potassium (K20) lakini sio
kiwango kinachotosheleza mahitaji haswa ya mbegu za mahindi zinapochipua. Nyunyuzia
P205 karibu na mbegu ili ziote kwa haraka. K20 hutumika kwa kiwango kikubwa lakini
hitaji la mimea hubainika baada ya upimaji wa hali ya udongo kujua kiasi cha mahitaji (soil
test). (ndo maana twasisitiza mbolea za viwandani sio lazima iwe ya chemical).
MBOLEA WAKATI WA KUPANDIA
Mbolea maarufu za kupandia katika soko la Tanzania ni: TSP, DAP, Minjingu Phosphate na Minjingu Mazao. Lakini zile ambazo zimechaguliwa kwenye mradi wa kukuza matumizi ya Minjingu Phosphate ni DAP, Minjingu Phosphate na Minjingu Mazao.
MBOLEA WAKATI WA KUKUZIA
Kwa matokeo bora, weka mbolea za kukuzia kama Urea, CAN ama SA. Kiwango cha urea ni nusu kizibo cha soda kwa kila shina. Mara nyingi mbolea hizi zinatoa kirutubisho cha naitrojeni. Urea inakirutubisho cha naitrojeni (N) kwa kiwango cha asilimia 46 na watu wengi wanauzoefu nayo.Vilevile bei yake ni nafuu ikilinganishwa na mbolea zingine za kukuzia. Mbolea hii iko katika hali ya chengachenga za mviringo (granules) za rangi nyeupe.
Dalili za mmea kukosa mbolea ni: Ukosefu wa K20 husababisha ncha za majani kuwa na rangi ya njano na kuunda gunzi (cob) lisilo na punje hadi juu. Ukosefu wa P205 hufanya matawi kuwa na rangi ya samawati na mbegu zisizo laini. Dalili za ukosefu wa nitrogen ni majani ya rangi ya manjano na mimea dhaifu mifupi.
UPALILIAJI & UNYEVU
Magugu yanaweza pia kuhifadhi wadudu na magonjwa yanayoweza kushambulia mimea iliyopandwa na hivyo kupunguza mavuno. Ni muhimu shamba lipaliliwe baada ya mimea kuota ili kuondoa magugu. Magugu ni mimea hivyo hushindana na mimea iliyopandwa na mkulima kwa kunyonya virutubisho vilivyoko katika ardhi.

MAGONJWA & WADUDU



MAGONJWA
1. Doa jani la kijivu la mahindi (Cercospora zeae-maydis & Cercospora zeina)
Doa jani la kijivu la mahindi umeibuka kama ugonjwa ulioweka kikwazo kwa mazao ya
mahindi nchini Marekani na kusini mwa Afrika katika miaka 25 iliyopita. Ingawa
ulidhaniwa kuwa aina moja ya kuvu, Cercospora zeae-maydis, ukaguzi wa chembechembe
umeonyesha kuwa kuvu lingine, C. zeina, hupatikana kwa wingi mashariki mwa Marekani
na kusini mwa Afrika. Mbegu za kuvu, zinazoishi katika mabaki ya mazao ya awali,
hurushwa na matone ya mvua kwenye majani ya chini ya mmea na kusababisha madoa
marefu yanayoungana kwenye mimea isiyohimili na kusababisha baka. Mashina
hudhoofika na kuanguka wakati wa mikurupuko ya magonjwa.
Kudhibiti: Ugonjwa unaweza kusimamiwa kwa kuharibu mabaki ya mimea baada ya kuvuna, kilimo cha mzunguko, kwa kutumia aina zinazovumilia ugonjwa zaidi, na, matumizi ya dawa za kuua kuvu ikiwa zitaleta faida kiuchumi.

2. Muozo wa mahindi na mycotoxin (Fusarium and Aspergillus species)
Kuna aina nyingi za kuvu zinazotokea kwenye mahindi na kuzalisha sumu za kikemikali
ambazo huchafua chakula na lishe. Zinajulikana kwa pamoja kama mycotoxins, na sumu
hizi zina madhara makubwa kwa afya ya binadamu na wanyama.
Aspergillus inasemekana kuwa mzalishaji muhimu zaidi wa mycotoxin katika Afrika,
ingawa kuvu nyingine kama vile Fusarium pia inahusika. Makundi yote mawili ya kuvu
hukua kwenye sehemu za mimea zilizokufa na zinazooza na kusababisha kuoza kwa
mahindi katika shamba. Huzalisha unga mwingi wenye mbegu za kuvu juu ya mahindi,
kabla na baada ya kuvuna, lakini pia inaweza kuwa bila kuzalisha koga lolote. Muozo wa
mahindi unaosababishwa na kuvu zinazozalisha mycotoxin hutokea kwa wingi zaidi wakati
mahindi yana matatizo na yanakua vibaya.
Kudhibiti: kuvuna kwa wakati muafaka na kukausha mahindi kabla ya kuyahifadhi. Aflasafe™, njia mpya ya kibiolojia ya kudhibiti Aspergillus, inatumika katika mashamba kabla ya mahindi kutoa maua na imeonyesha matumaini makubwa katika kupunguza uchafuzi wa mahindi kabla ya kuvuna na baadaye mkusanyiko wa mycotoxins katika bidhaa zilizohifadhiwa.

3. Ugonjwa wa maize lethal necrosis (Multiple virus infections)
Maize lethal necrosis disease (MLND) ni ugonjwa mpya wa virusi barani Afrika.
Umesababisha wasiwasi mkubwa kwa sababu mimea hufa na hakuna nafaka au ni nafaka
kidogo tu zinazozaliwa.
Chanzo cha ugonjwa
Wataalamu katika tafiti zao wanasema kuwa, ugonjwa huu husababishwa na virusi vya aina
mbili vinavyoathiri mmea wa mahindi kwa pamoja ambavyo ni Maize Chlorotic Mottle
Virus (MCMV) na Sugarcane Mosaic Virus (SCMV).
Virusi hivi husambazwa na wadudu wa aina mbili, ambao ni Thrips pamoja na Aphids, japo
kuna wadudu wengine wanaweza kubeba na kusambaza ugonjwa huo kama vile beetles
and leafhoppers pamoja na matumizi ya mbegu zilizoathirika.
Dalili za mahindi yalioathirika
– Majani machanga ya juu hugeuka na kuwa na rangi ya njano na hatimaye kukauka
kuanzia pembezoni mwa jani kuelekea katikati na hatimaye mmea kufa.
– Mmea huweza kutoa machipukizi mengi sana.
– Mbelewele hukosa chamvua hivyo mmea kutozaa.
– Mahindi yakishambuliwa wakati yanajaza mbegu, gunzi husinyaa na kuweka mbegu
chache au kutojaza kabisa.
– Mahindi yaliyoathirika hushambuliwa na magonjwa nyemelezi hasa ukungu.
– Kwa mimea iliyoanza kusinyaa, huonyesha dalili za kukomaa kabla ya wakati, huku
hindi likiwa katika hali ya kuchoma maganda na kuonesha utayari wa kuvunwa.
Aidha, ugonjwa huo unaposhambulia katika hindi lililokomaa, basi huingia moja
kwa moja katika kiini cha punje.
Mahindi yaliyoathiriwa na ugonjwa huu huota fangas ambayo wataalamu wanasema
ina sumu kali ijulikanayo kama Aflatoxin. Sumu hiyo, husababisha madhara kwa
binadamu na wanyama.

Utafiti: Utafiti uliofanywa na wataalamu mbalimbali wakiwepo wataalamu kutoka Taasisi ya utafiti wa Kilimo ya Seliani (SARI) wamebaini kuwa, sumu hiyo (Aflatoxin) inayotokana na
fangasi, husababisha ugonjwa wa saratani ya ini kwa binadamu na wanyama. Utafiti huo
pia unaeleza kuwa, ugonjwa huo unaweza usionekane kwa haraka na huweza hata
kuchukua muda wa mwaka ndipo kujitokeza.
Hivyo basi, ni lazima mataifa yote kuwa makini na kuchukulia jambo hili kwa uzito zaidi.
Mbinu za kuepuka ugonjwa huu
• Panda mbegu bora zilizothibitishwa na Taasisi ya Uthibiti wa Ubora wa Mbegu (TOSCI)
nchini.
• Usipande mbegu zilizovunwa msimu uliopita kutoka katika shamba lililoshambuliwa na
ugonjwa.
• Safisha shamba kwa kuondoa magugu na masalia yote ya mazao na
kuyachoma/kuyafukia kuepuka maficho ya wadudu na virusi vya ugonjwa. Kagua shamba
mara kwa mara na kama utaona dalili zilizotajwa hapo juu, toa taarifa kwa mtaalamu wa
kilimo aliye karibu nawe.
Kudhibiti
• Ng’oa mapema mahindi yote yaliyoathirika, na kuyateketeza haraka.
• Usipande mahindi katika shamba lililoathirika angalau kwa msimu mmoja. Panda mazao
mengine kama vile viazi mviringo, mihogo kama utakavyoshauriwa na mtaalamu wa
kilimo.
• Katika maeneo yenye ugonjwa, dhibiti wadudu wasambazao ugonjwa huo kwa
kunyunyizia kiuatilifu kulingana na maelekezo ya mtaalamu.
• Zingatia kilimo cha mzunguko wa mazao na toa taarifa mapema kwa afisa ugani wa kilimo
endapo utaona dalili za ugonjwa.
Ugonjwa wa MLND bado unafanyiwa utafiti kwa undani zaidi na dawa bado haijapatikana.
Hivyo wakulima wote wanatakiwa pindi wanapoona kuna dalili zozote zimeanza kujitokeza
katika mashamba yao, hawana budi kung’oa mimea yote bila kujali kama mengine
hayajaambukizwa kasha waziteketeze kwa moto. Hii ni kutokana na sababu kuwa hata
mimea ambayo bado haijaonesha dalili za kuambukizwa, hana budi kuonesha dalili
mapema kwani maambukizi husambaa kwa kasi sana na kwa muda mfupi.

4. Ugonjwa wa matupa kwenye mahindi (SMUT).
Ugonjwa huu hushambulia sehemu za uzazi za mahindi. Mashambulizi hufanywa na aina
mbili za vimelea jamii ya uyoga (ukungu) vijulikanavyo kwa majina ya kitaalamu
kama Sphacelotheca reliana na Ustilago maydis. Vimelea hivyo husababisha magonjwa ya
aina mbili ambayo dalili zake zinafanana. Mimea iliyoshambuliwa na ugonjwa huu ama
haizai kabisa ama inazaa kiasi kidogo ukilinganisha na jinsi ambavyo ingeweza kuzaa kama
isingekuwa imeshambuliwa. Kwa hiyo mashambulizi ya magonjwa haya husababisha
hasara ya mavuno.
Inakadiriwa kwamba hasara ya mavuno inawezakuwa kidogo tu ama asilimia kumi (10%)
au hata zaidi ya kiwango hicho, lakini kupoteza ni kupoteza hata kama ni kiwango kidogo.
Ugonjwa wa “matupa” unaosababishwa na kimelea kijulikanacho kama Ustilago
maydis hufahamika kama “Common Smut” kwa kiingereza.
Dalili zake huwa kuota kwa uvimbe katika sehemu za mmea zinazokua kama vile punje za
mahindi, mbelewele na hata kwenye majani. Uvimbe huo ukikauka na kupasuka hutoa
vumbi jeusi kama masizi ambayo ndiyo viini vya/mbegu ya huo ugonjwa. Dalili ya msingi
ya ugonjwa huu kwenye mhindi ni kwamba inawezekana kuwa na baadhi ya punje
zilizoshambuliwa na zingine ambazo hazina dalili katika gunzi moja.
Ugonjwa wa “smut” unaosababishwa na kimelea kijulikanacho kwa jina Sphacelotheca
reliana hufahamika kama “Head smut” kwa kiingereza. Kama ilivyo kwa ugonjwa wa
“smut” ya kawaida, dalili za ugonjwa huu hujitokeza mara nyingi katika hindi lenyewe na
mbelewele na mara chache katika shina la mhindi. Tofauti na ugonjwa wa “smut” ya
kawaida, katika ugonjwa huu badala ya mhindi kuathiriwa baadhi ya punje, hindi zima
hujaa vumbi jeusi ndani ambapo kwa nje ni kama mfuko mweupe ambao kabla ya kukauka
hufana na uyoga. Vumbi hilo jeusi ndilo viini vya kimelea. Vivyo hivyo kwenye mbelewele.
Wakati mwingine mmea ulioshambuliwa na ugonjwa huu hudumaa na hushindwa kuzaa.
Dalili nyingine ya ugonjwa huu ni mhindi kuotesha vijani vidogo badala ya mbelewele.
Udhibiti wa Ugonjwa wa “SMUT”
1. Tumia mbegu bora ingawa mpaka sasa haipo mbegu maalumu yenye kustahimili
ugonjwa huu. Kwa kutumia mbegu bora, mkulima utajihakikishia mavuno bora.
2. Daima hakikisha unalima kilimo cha kisasa kikijumuisha urutubishaji wa udongo.
Epuka kuijeruhi mimea uwapo shambani. Mimea iliyo na majeraha hushambuliwa kwa
urahisi na ugonjwa huu. Pia dhibiti wadudu waharibifu ambao pamoja na
madhara mengine wanayosababisha pia huijeruhi mimea na kwa hivyo kurahisisha
maambukizo ya ugonjwa huu wa “smut”.
3. Kila inapowezekana tumia kilimo cha kubadilisha mazao. Katika kubadilisha mazao ni
vema kutumia mzunguko wa mazao yasiyoshambuliwa na ugonjwa wa “smut” kama vile
ngano, shayiri, njegere, viazi na maharagwe.
4. Unapolima hakikisha masalia mabua yamefukiwa chini sana.

WADUDU
1. Vipekecha shina wa mahindi (Busseola fusca; Chilo and Sesamia species)
Vipekecha shina wa mahindi ni wadudu waharibifu wa mahindi, mtama na mazao mengine
katika nchi nyingi za Afrika. Viwavi wa nondo, huchimba na kuingia ndani ya shina la
mahindi, wakila tishu za ndani na kusababisha mmea kunyauka na hatimaye kufa.
Wadudu hao wanaweza kudhibitiwa kwa njia mbalimbali kama mbinu za kitamaduni, hasa,
kilimo cha mseto na mfumo wa ‘sukuma-vuta’ (‘pushpull’). Pia wanaweza kudhibitiwa na
dawa za kuua wadudu, unga wa mwarobaini, lakini katika hatua za mapema, kabla ya
mabuu kuchimba na kuingia ndani ya shina.

2. Osama (Prostephanus truncates)
Dumuzi ‘Osama’ ni mdudu hatari sana wa mahindi ya kuhifadhiwa kote barani Afrika.
Osama hula ndani ya nafaka na kuacha shimo na ganda tupu. Ghala safi ya kuhifadhia ni
muhimu ili kuweza kuzuia uharibifu wa osama. Kukoboa nafaka kutoka kwa gunzi kabla ya
kuhifadhi kunaweza kupunguza uharibifu.

3. Funza wa vitumba (Helicoverpa armigera)
Funza wa vitumba ni mdudu msumbufu wa mimea mingi muhimu ya chakula, mafuta na
fedha duniani kote, ikiwa ni pamoja na nafaka mfano Mahindi ikiwa ni mojawapo, mikunde,
matunda na mboga. Ushambulizi mkali wa viwavi wa nondo huyu kunaweza kusababisha
hasara kwa mavuno yote.
Kudhibiti: kwa njia ya kemikali kunapaswa kufanywa kwa makini na wakati mwafaka kwa
kuwa viwavi hutoboa na kuingia ndani ya nafaka au matunda ya mmea, hivyo kuweza
kulindwa. Usugu kwa dawa, kama vile za pyrethroid, kumeripotiwa katika nchi nyingi.
Bakteria aina ya Bacillus thuringiensis (Bt) na madawa ya mwarobaini hutoa udhibiti wa
ufanisi dhidi ya viwavi na wakati huo huo kupunguza uharibifu wa maadui wa kiasili.
Udhibiti muhimu wa kitamaduni ni pamoja na kuondoa na kuharibu mabaki ya mimea
baada ya kuvuna, kulima udongo ili uwatoe nje pupae na kupanda kwa wakati mmoja.

UVUNAJI
Uvunaji hufanyika kwa kutumia mikono kwa mashamba madogo na mashine (combine
harvester) hutumika kwa ajili ya mashamba makubwa, Zao la wastani la mahindi
ulimwenguni mnamo mwaka 2000 lilikuwa kilogramu 4255 kwa kila hekta. Zao la wastani
nchini Marekani ilikuwa kilo 8600 kila hekta, huku mataifa yaliyo chini ya jangwa la Sahara
la Afrika yakivuna kilo 1316 kwa kila hekta ya shamba.
Zao la wastani katika taifa la Tanzania kati ya mwaka 2001-2005 lilikuwa kati ya gunia
15-19 kwa hekta (sawa na kilo 1350-1750) Ukilima kwa kuzingatia ukulima wa kisasa na
kanuni zake kwa Tanzania utavuna kilo 5000 kwa hecta (ukanda wa pwani) na kilo 7500
kwa nyanda za juu kama Iringa, Mbeya, Ruvuma, Arusha n.k


Contact/ Wasiliana nasi
Phone (Simu): +255766797400 Email: daudilyela@yahoo.com

Our Services ( Huduma zetu): Research( Utafiti), Project Proposal ( Mapendekezo ya Miradi), Business Plan ( Plani za Biashara), Profit Assessment ( Upimaji wa Faida),

No comments:

Post a Comment

KILIMO BORA CHA NDIZI

Ndizi ni tunda muhimu Afrika ya Mashariki na katika nchi za joto kwa jumla hasa visiwa vya caribian. Mmea wake huitwa mgomba. Kibiolojia n...